HII NDIO HUKUMU YA ASKARI ALIYE MUUA MWANGOSI IRINGA
MAHAKAMA kuu kanda
ya Tanzania kanda ya Iringa imemhukumu kwenda jela miaka 15 askari Polisi Kikosi cha Kutuliza
Ghasia ( FFU )Iringa namba G 58 police constable Pacificius
Cleophace Simon (27) kwa kosa la kumuua bila kukusudia
mwaahabari Daudi
Mwangosi mwaka 2012 katika kijiji
cha Nyololo wilaya ya
Mufindi. wakati akiwa katika majukumu yake ya kuchukua
habari huku mke wa marehemu Mwangosi Itika Mwangosi akipongeza
vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano mkubwa katika kufuatilia
kesi hiyo. .
"Mahakama
inatambua uchungu wa familia iliyoupata kwa kifo cha marehemu
Daudi Mwangosi ambaye aliuwawa pia marehemu aliuwawa kikatili
....siku zote adhabu inapaswa kulingana na kosa husika mahakama
haiafiki maombi ya wakili wa upande wa utetezi kuomba mshtakiwa
apewe adhabu ya kuachiwa huru kwa kuwa ni yatima ....mgongano wa
hisia umeonekana katika kesi hii ila mahakama inampa adhabu ya
kwenda jela miaka 15" alisema jaji Dkt Paul Kiwelo
Akisoma
shauri ya kesi hiyo kabla ya kutoa adhabu leo mahakamani hapo
jaji Dkt Kiwelo aliwashukuru wazee wa baraza la mahakama kwa
michango yao mkubwa mchango ulioisaidia mahakama hadi kufikia
siku hiyo ya hukumu pia mawakili wote walioshiriki katika kesi
hiyo.
"
Suala la aina gani ya adhabu inafaa halikuwa rahisi sana kwani
shauri hili upande wa jamhuri uliomba adhabu ya kufungwa
maisha jela huku upande wa utetezi ukiomba mshitakiwa aachiwe huru
kwa masharti ambayo mahakama ingeona yanafaa kutokana na kuwa na
majukumu ya kulea wadogo zake na yeye kuwa yatima .....mahakama
imetazama ukubwa wa kosa husika pia jamii ina mtazamo gani
katika kesi hiyo lakini mahakama haitoi hukumu kwa mitazamo mbali
mbali inatumia vifungu vya sheria suala la kutoa adhabu ni la
kisheria si vinginevyo"
Jaji
Dkt Kiwelo alisema kuwa adhabu haitolewi kwa ajili ya kulipiza
kisasi ila inatolewa kama sehemu ya onyo na kuifanya jamii
kutambua kuishi kwa kuheshimu misingi ya sheria kwani kuna
mambo manne katika kesi yanatazamwa likiwemo la medhania ya kosa
alilotenda na aina ya kosa pia maslahi ya jamii katika kosa
husika.
"Naomba
kusema mgongano wa hisia umeonekana katika kesi hii pamoja na
kuwepo kwa changamoto hizo bado mahakama haijayumbishwa na migogano
hiyo .....mahakama haiitoi hukumu kwa kutazama ni kosa la kwanza
wala mhusika hana rekodi mbaya ya makosa mahakama inaendeshwa kwa
sheria ndugu wangefurahi kuona mtuhumiwa anafungwa hivyo siafiki
maombi ya upande wa utetezi juu ya mkosaji naamini kabisa kwa
kosa hili kumwachia kwa Masharti haki haitakuwa imetendeka"
Kwa
mujibu wa sheria kuua bila kukusudia ni kosa kubwa sana ambapo
adhabu yake huwa ni kufungwa jela maisha japo kila kosa
huamuliwa kutokana na mazingira yake hivyo lazima upewe adhabu
ambayo itakuwa funzo kwa wengine.
"
Kuua si jambo dogo na mahakama hii kwa kuzingata vifungu vya
sheria na pia mtuhumiwa umekaa mahabusu miaka minne inakuhukumu
kwenda jela miaka 15 rufaa ipo wazi kwa asiyeridhika"
Akizungumza na wanahabari mara baada ya hukumu hiyo aliyekuwa wakili wa utetezi Lwezaula Kaijage alisema kuwa alisema kuwa yeye alikuwa ni wakili wake na kuwa kwa sasa hawezi kusema ni uamuzi gani ambao mteja wake anaweza kuchukua hadi hapo atakapowasiliana nae
"
Nafikiri wote mlikuwepo mahakamani mmesikia kuwa amefungwa miaka
15 itabidi sasa mimi niende magereza kuzungumza nae ili nichukue
sheria nione zinasemaje pia kuomba mwenendo mzima wa sheria kuona
jinsi ulivyokwenda ili nione ni kitu gani ambacho labda
mahakama ilielekezwa vibaya kabla ya kutoa hukumu hiyo kama
nitaona kuna jipya basi tutakwenda kwenye rufaa"
Wakili wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu ((THRDC)Benedict Ishabakaki alisema kuwa katika hukumu hiyo mahakama kuu kanda ya Tanzania kanda ya Iringa imetenda haki pasipo kuegemea upande wowote na kuwa pamoja na nguvu kubwa ya polisi na jinsi ambavyo ushahidi uliokuwa umepelekwa kulenga kumnasua mwenzao ila mahakama hiyo imetumia ushahidi wa ungamo la mlinzi wa amani kutoa hukumu ambayo kimsingi haijaacha maswali kwa wananchi .
Wakili
Shabakaki alisema kuwa kesi hiyo polisi waliifanya kama kesi ya
nyani kumhukumu ngedele kwa kula mahindi kwani alisema aliyetenda
kosa alikuwa ni askari ,mchunguzaji wa kesi hiyo ni askari hivyo
katika mazingira hayo haikuwa rahisi kesi hiyo kufikia hukumu hiyo
ila mahakama imetenda haki na kuwa wao kama watetezi wa haki za
binadamu wataona ni hatua zipi za kuchukua baada ya mahakama
kutenda haki .
Alisema
pamoja na jukumu la polisi la ulinzi wa jamii ila polisi baadhi yao
wameendelea kukiuka wajibu wao na kuogopwa zaidi na raia jambo
ambalo si jema na kuwa nguvu kubwa iliyotumika siku zote wakati
wa kesi hiyo ni kielelezo tosha kuwa polisi walikuwa wakitegemea
mwisho wa siku mwenzao huyo kuachiwa huru .
Rais
wa Umoja wa Klabu
za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema kuwa wao
kama UTPC wanapongeza mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa kwa
kutenda haki katika kesi hiyo kwani alisema kuwa jeshi la polisi
walipanda kuharibu kesi hiyo ila jaji kwa umakini wake ametoa
adhabu
"
Sisi kama wanahabari tunajipongeza pia kwa hukumu hii kwanza kutiwa
hatiani kwa mtuhumiwa na pili kufungwa jela miaka 15....... na
ifahamike kuwa kesi hiyo ilikuwa ikiihusu serikali hivyo hukumu
ya kesi hiyo imeingia katika rekodi ya dunia kuwa mwandishi
aliuwawa na muuaji amefungwa miaka 15 jeshi la polisi Iringa kwa
muda wote limekuwa likiwanyanyasa waandishi hivyo sisi kama
viongozi wa wanahabari tutakwenda kuonana na viongozi wao wa juu"
Alisema
kuwa yapo mambo ya msingi ambayo jeshi la polisi linapaswa kufanya
ila si kwa kutumia nguvu kubwa kunyima uhuru wa vyombo vya habari
hasa katika kesi hiyo ya Mwangosi .
"
Polisi katika kesi nyingine wamekuwa wakiwasaidia wanahabari
kupata picha kirahisi kwa watuhumiwa pindi wanapofikishwa
mahakamani ila katika kesi hiyo wamekuwa wakimfunika mwenzao na
kuzuia waandishi kupiga picha ila pamoja na yote hayo adhabu
imetolewa pale pale"
Makamu
Mwenyekiti wa
Jukwa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile alisema kuwa polisi
Iringa walitamani kuona kesi hiyo inaharibika na kama
lisingelikuwa ungamo la mlinzi wa amani mtuhumiwa huyo alikuwa
anaachiwa huru na ungamo chini ya mlinzi wa amani ni mahakama
yenyewe hivyo ni wazi mahakama imeweza kutenda haki zaidi .
"
Adhabu ni kumfanya mtu ajirekebisha na wapo waliotegemea kuwa
muuaji wa Mwangosi nae ana hukumiwa kufa ila si haki binadamu
....lakini mtuhumiwa huyo wakati wote wa kesi hiyo hakupaswa
kufikishwa mahakamani na polisi wenzake badala ya askari wa magareza
ambao ndio wanawajibu wa kumpeleka mahakamani na mahabusu ila
.....hata leo baada ya hukumu hatujui amepelekwa wapi maana
wameondoka nae wao wenyewe ambao walitaka kesi ivurugike sasa
sijui wanampeleka rumande ama gerezani au wamempeleka nyumbani
kwanza kula chakula lakini naomba hili kuliacha hapo"
Bw
Balile alisema
kuwa kwa sasa wanaanzisha mchakato wa kufungua kesi ya madai kwa
ajili ya familia ya Mwangosi na kuwa kujua ni mahakama ya ndani ama
ya Afrika ambayo kesi hiyo itafunguliwa itajulikana baada ya kwenda
kukaa na viongozi wenzake japo alisema haki yote itafikishwa kwa
familia ya Mwangosi
Juzi
Julai 25 mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa ilimkuta na hatia
askari Simon katika kesi hiyo namba 45 ya mwaka 2013 ya mauaji ya
bila kukusudia ya
mwahabari
Mwangosi aliyeuwawa kinyama Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji
cha Nyololo wilaya ya
Mufindi wakati chama cha Demokrasia na maendeleo (chadema)
wakifanya uzinduzi wa matawi huku kukiwa na katazo la matukio ya
mikutano ama mikusanyiko ya kisiasa kutokana na serikali kuongeza
muda wa kuendelea na zoezi la senza ya watu na makazi.
Mjane
wa marehemu Mwangosi Bi Itika Daudi Mwangosi alitoa pongezi
nyingi kwa wanahabari kwa ushirikiano wao wakati wote wa kesi
hiyo hadi ilipofikia mwisho .
"
Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutufikisha salama siku hii ya leo .....na niishukuru mahakama kuu
ya Tanzania kanda ya Iringa kwa kuweza kutenda haki pili
ninawashukuru sana ninyi waandishi wa habari kwa umoja wenu
...nawashukuru sana tena sana zaidi ya sana hata kama mtu
amekutendea wema gani Mungu alitupa neno moja tu la ahsante pia
napenda kuwatia moyo msiogope songeni mbele Mungu yu paoja nanyi
kama alivyowapigania hadi kufika leo atazidi kuwapigania zaidi
teteeni kazi zenu elimisheni jamii vile mnavyoendelea kusaidia
jamii ndivyo Mungu anavyowabariki daima sina neno la zaidi zaidi ya
ahsante "